Soka Ufukweni:Tanzania, Misri kupambana

Image caption Timu ya Taifa ya Soka la ufukweni ya Tanzania

Timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni (Beach Soccer) inatarajiwa kucheza na timu ya Taifa ya Misri siku ya ijumaa majira ya saa 10 kamili jioni, mchezo utakofanyika katika klabu ya Escape 1 Msasani jijini Dar es salaam.

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kinaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo huo, ambapo kwa takribani wiki mbili kipo kambini Bamba Beach wakijifua kwa mchezo huo.

Tanzania ilifuzu hatua ya pili baada ya kuiondoa timu ya Taifa ya Kenya kwa jumla ya mabao 12 -9, na endapo itafanikiwa kuwaota Misri, itafuzu moja kwa moja kucheza Fainali za soka la Ufukweni zitakazofanyika Visiwa vya Shelisheli mwezi April mwaka huu.

Waamuzi wa mchezo huo ni Eid Haitham Eid Hassan (Sudan), mwamuzi msaidzi wa kwanza Abaker Mohamed Bilal (Sudan), mwamuzi msaidizi wa pili Abdalla Hassain Hassaballa, mtunza muda (time-keeper) Boubaker Bessem (Tunisia) wakati kamisaa wa mchezo huo ni Khiba Herbert Mohoanyane kutoka Lesotho.

Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini Misri kati ya Machi 20,21 na 22 mwaka huu.

Kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu , Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), inaitakia kila la kheri na ushindi timu ya Taifa ya soka la ufukweni (Beach Soccer) katika huo dhidi ya Misri.