Al Ahly ni mabingwa wa Afrika wa Voliboli

Image caption Al Ahly ilishinda bingwa mtetezi Esperance ya Tunisia seti 3-1 katika mechi ya fainali ya mashindano ya voliboli ya klabu bingwa Afrika

Al Ahly ilishinda bingwa mtetezi Esperance ya Tunisia seti 3-1 katika mechi ya fainali ya mashindano ya voliboli ya klabu bingwa Afrika kwa wanaume mjini Sousse, Tunisia, Jumatatu usiku wiki hii.

Kwa ushindi huo hii ni mara ya kumi na moja Al Ahly imeibuka mshindi kwenye mashindano haya, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka wa 1980.

Etoile du Sahel ya Tunisia ilimaliza ya tatu na kujituliza na medali ya shaba baada ya kushinda Somoha ya Misri seti tatu-sifuri huku timu za Kenya Magereza na GSU zikiongoza eneo la Afrika Mashariki na Kati...

Al Ahly ilianza mechi ikitumia sana wazuiaji wao wa kati haswa Abdel Halim Fahim ambaye alikuwa mchezaji mrefu zaidi kwenye mashindano hayo.

Image caption Al Ahly ilishinda bingwa mtetezi Esperance ya Tunisia seti 3-1

Ahly ilishinda seti ya kwanza 25-19 na Esperance ikashinda ya pili 26-24 kisha Ahly ikanyamazisha Esperance kwa kushinda seti ya tatu na ya nne 25-18,25-19..

Bingwa mara tano Zamalek ya Misri ilimaliza ya tano kwa kuichapa Ittihad Tangier ya Morocco seti 3-0 na Borj Bouririj ya Algeria ikawa ya sita ikifuatiwa na Ittihad Tangier ya Morocco, Setif ya Algeria, FAR ya Morocco na Ahly Beni Ghazi ya Libya katika nafasi ya kumi..

Sweli ya Libya ilimaliza ya 11 kwa kuishinda Magereza ya Kenya seti 3-2. Timu hiyo ya Kenya ilionyesha mchezo mzuri na kuisukuma vilivyo Sweli..

Magereza ilichukua na nafasi 12 na ikaongoza kwa timu za Afrika Mashariki na Kati ikifuatiwa na timu nyingine ya Kenya GSU iliyomaliza ya 13 kwa kushinda Espoir ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo seti 3-1.

Image caption Etoile du Sahel ya Tunisia ilimaliza ya tatu

Autoridade ya Msumbiji ilimaliza ya 14 ikifutaiwa na AS Douanes ya Burkina Faso, FAP ya Cameroon, APR ya Rwanda katika nafasi ya 18, Kampala AVC ya 19 kisha Support United ya Zimbabwe halafu Al Nahda ya Sudan ikavuta mkia nafasi ya 21.

Wakati huo huo, mechi ya kwanza ya robo-fainali ya mashindano ya kriketi ya kombe la dunia itafanyika Jumatano wiki hii mjini Sydney, Australia kati ya Afrika Kusini na Sri Lanka.

Mechi ya pili Alhamisi ni kati ya bingwa mtetezi India dhidi ya Bangladesh mjini Melbourne kisha Ijumaa Australia inatoana jasho na Pakistan na Jumamosi New Zealand dhidi ya West Indies.

Mechi za nusu-fainali ni Machi tarehe 24 na 26 na fainali ni Machi tarehe 29.