Man City watolewa ligi ya mabingwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Barcelona na Manchester city

Timu za England zimetolewa katika kinyang'anyiro cha michuano klabu bingwa barani Ulaya,baada ya Man City kuchabangwa bao 1-0 dhidi ya Barcelona na kuondolewa katika mashindano hayo, ilikuwa zamu ya Manchester City kufuata nyayo za waingereza wenzao kutupwa nje ya mashindano na miamba ya soka ya Hispania Barcelona. Katika kipute hicho kilichopigwa katika dimba la Nou Camp.

Wenyeji Barcelona walijipatia bao lao katika dakika ya 31 baada mchezaji Ivan Rakitic kuitumia vema pasi maridadi kutoka kwa Leonel Mess. Hadi mwisho wa mchezo Barcelona 1 Man City hawakupata kitu na kufanya jumla ya matokeo kuwa ni 3-1 baada ya mchezo wao wa awali vijana wa Manuel Pellegrini kuanguka nyumbani kwa jumla ya mabao 2-1.

Na huko nchini Ujerumani vijana wa Jurgen Klopp Borussia Dotmund, ilikiona cha moto baada ya kutandikwa bao 3 kwa mshangao dhidi ya Juventus ya Italia,katika mtanange huo uliopigwa katika dimba la Sigunal Iduna Park, mchezaji Carlos Tevez ndiye aliyepeleka msiba kwa Wajerumani hao kwa kutumbukiza kimiani mabao mawili. Dakika tatu tu za mchezo huo zilimtosha Tevezi kufunga bao la kuongoza kabla ya Morata kuandika bao la pili dakika ya 70 na kisha Tevez kutikisa tena nyavu katika dakika ya 79. Matokeo ya jumla kati ya timu hizo mbili yanakuwa ni 5-1 baada ya Juventus kushinda 2-1 katika mchezo wa awali.