Kriketi:India imefuzu kwa nusu-fainali

Haki miliki ya picha Getty
Image caption India leo hii imefuzu kwa nusu-fainali ya mashindano ya kriketi ya kombe la dunia kwa kushinda Bangladesh mjini Melbourne

India leo hii imefuzu kwa nusu-fainali ya mashindano ya kriketi ya kombe la dunia kwa kushinda Bangladesh mjini Melbourne

kwa mikimbio 109 na sasa itakutana na mshindi wa mechi ya Ijumaa wiki hii ya robo-fainali kati ya Pakistan na Australia.

Wadadisi wengi wanasema wangetaka sana mechi ya India na Pakistan ama Australia iwe fainali lakini sasa hii itakua fainali kabla ya fainali kwani mataifa yote ni miamba kwenye mchezo huu wa kriketi...

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wachezaji wa timu ya India

India kufikia sasa wameshinda mechi 11 mfululizo, na kwa ushindi wao leo hii nyota alikuwa ni Rohit Sharma aliyepata mikimbio 137 kwa mipira 126.

India ilishinda urushaji wa sarafu na ikaamua kupiga mwanzo na kupata mikimbio 302 kwa sita.

Na hapo ikawa ni dhahiri kwamba Bangladesh wana mlima wa kupanda kufikia mikimbio 303 kuibuka mshindi wa mechi hii ya robo-fainali.

Kama ilivyotarajiwa Bangladesh, ambao walishiriki robo-fainali ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza, waliangamizwa bila tatizo na India.

Haki miliki ya picha GETTY IMAGES
Image caption Mashabiki wa kriketi kutoka India

Wakapata mikimbio 193 pekee kwa overs 45 huku wapigaji wao wote wakiwa wametolewa.

Afrika Kusini ndio ilifuzu mwanzo kwa nusu-fainali Jumatatu wiki hii ilipoicharaza Sri Lanka kwa wiketi tisa kwenye mechi ya robo-fainali.

Afrika Kusini sasa itakutana na New Zealand ama West Indies ambao watacheza mechi yao ya robo-fainali kesho kutwa katika uwanja wa Wellington, New Zealand.