Afrika na Blatter uraisi FIFA

Image caption Sepp Blatter

Afrika imesisitiza msimamo wake wa kumchagua Sepp Blatter katika nafasi ya urais katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa miguu duniani (FIFA) hapo mei mwaka huu.

Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga,ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) amesema Cecafa na nchi za Afrika kwa ujumla wamekubaliana kumchagua Blatter.

Tenga amezungumzia msimamo wa bara la Afrika uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa CAF uliofanyika mwaka jana jijini Sao Paulo, Brazil kuwa wanachama wote wa CAF watamuunga mkono Rais wa sasa wa FIFA anayetetea nafasi yake katika uchaguzi utakaofanyika Mei mwaka huu jijini Zurich, Uswisi.

Vilevile Mkutano Mkuu wa CECAFA uliofanyika Desemba 2014 jijini Nairobi, Kenya ulipitisha azimio la kumuunga mkono Joseph Sepp Blatter katika uchaguzi wa FIFA.

Blatter amekuwa akiungwa mkono na nchi za Afrika kwa sababu analipa kipaumbele bara la Afrika katika maendeleo ya mpira wa miguu, ikiwemo nafasi iliyoipata Afrika ya kuandaa kombe la Dunia na kuweka historia kubwa duniani mwaka 2010 nchini Afrika ya Kusini.

Uamuzi huo wa Afrika, endapo utafanikiwa, utakuwa ni pigo kwa mchezaji wa zamani wa klabu tajiri zaidi duniani, Luis Figo, raia wa Ureno ambaye pia ametangaza nia ya kugombania nafasi hiyo kubwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, katika mkutano ulioitishwa na Tenga, rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi pia amesema Tanzania inamuunga mkono Blatter.

Rais Tenga ameishukuru familia ya TFF kwa kumuunga mkono katika kugombea tena nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 7 mwaka huu Cairo.

Tenga ni mgombea pekee wa nafasi hiyo kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.