Twiga Stars kuikabili She-polopolo

Image caption Twiga Stars ya Tanzania

Timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwakarisbisha timu ya taifa ya wanawake ya Zambia 'The She-Polopolo'.

Twiga Stars inayonolewa na kocha mkuu Rogasian Kaijage imeingia kambini na kikosi cha wachezaji 25 kujiandaa na mchezo huo ambao ni muhimu wa kuwania kufuzu kwa fainali za michezo ya Afrika mwaka huu.

Katika mchezo wa awali uliofanyika wiki mbili zilizopita jijini Lusaka Zambia, Twiga Stars iliibuka na ushindi wa mabao 4-2, mabao yaliyofungwa na Asha Rashid (2), Shelder Boniface (1) na Sophia Mwasikili (1).

Mshindi wa jumla katika mchezo huo atafuzu moja kwa moja kwa fainali za Michezo ya Afrika zitakazofanya nchini Congo - Brazzavile kuanzia Septemba 13 mwaka huu.