Chelsea yashinda huku Costa akijeruhiwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Diego Costa akianguka katikakati ya wachezaji wa stoke city

Mkufunzi wa kilabu ya Chelsea Jose Mourinho amesema kuwa ilikuwa hatari kumchezesha mshambuliaji Diego Costa baada ya kujeruhiwa wakati wa ushindi wa Chelsea wa 2-1 dhidi ya kilabu ya Stoke City siku ya jumamosi.

Costa alichukua mahala pake Oscar wakati wa mapumziko huku mabao yakiwa 1-1, lakini alicheza kwa dakika 10 pekee kabla ya kulazimika kutoka nje baada ya kupata jeraha jengine.

''Kama matokeo yangalikuwa 2-0 asingecheza.Lakini ilibidi tumchezesha .Kitengo changu cha matibabu kiliamua kumchezesha'', alisema Mourinho.

Amsema kuwa mshambuliaji huyo atakuwa nje kwa wiki mbili .

Hii inamaanisha kwamba Costa ataikosa mechi dhidi ya QPR tarehe 12 mwezi Aprili na ile dhidi ya Manchester United katika uwanja wa Stamford Bridge tarehe 18 mwezi Aprili.