Mancity yawalenga nyota 3 wa Liverpool

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Coutinho

Manchester City imemuorodhesha Phillipe Coutinho kama mchezaji wa tatu wanayepanga kumnunua kutoka kwa mahasimu wao Liverpool.

Timu hiyo tajiri inapanga kutumia mamilioni ya fedha kuwanunua wachezaji wapya mwishoni mwa msimu huu kufuatia matokeo mabaya.

Mabingwa hao wanapanga kukibadilisha kikosi hicho hatua ambayo huenda ikawakosesha taji lolote.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Raheem Sterling

Mwenyekiti Khaldoon Al- Mubarak ameandika majina ya baadhi ya wachezaji wakiwemo nyota wa England Raheem Sterling na Jordan Henderson.

Imebainika kuwa kilabu hiyo pia inapanga kumnunua mchezaji wa Brazil Coutinho.

Inadaiwa kuwa wakuu wa kilabu hiyo wanaamini Coutinho anaweza kuhamishwa hadi katika uwanja wa Etihad kwa kitita sha pauni millioni 20 iwapo Liverpool itashindwa kuorodheshwa miongoni mwa timu nne bora zitakazofuzu kucheza katika kombe la vilabu bingwa Ulaya.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jordan Henderson ni miongoni mwa wachezaji wanaolengwa na Mancity

Habari hizo huenda zikamshtua Brendan Rodgers ambaye anawaona wachezaji wake wakiwindwa na kilabu pinzani.

Rodgers angependa sana kuwazuia wachezaji wake katika uwanja wa Anfield lakini pia anajua kwamba hawezi kushindana na mfuku mzito wa mmiliki wa kilabu hiyo Sheikh Mansour.