Taifa stars ya Tanzania yajinasibu

Image caption Kocha wa Taifa Stars Mart Nooij

Licha ya kupangwa katika kundi gumu na timu za Nigeria, Misri na Chad katika michuano ya kuwania kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika 2017 nchini Gabon, kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mdachi Mart Nooij amesema timu yake haiziogopi timu hizo.

Ameongeza kuwa badala yake, zitegemee pia upinzani mkali kutoka kwa Stars ambayo ana amini itakuwa imejiandaa vema kwa ajili ya mashindano hayo ambapo kushinda, kufungwa au kupata sare itakuwa ni sehemu ya matokeo.

Michuano ya Cosafa itakayofanyika nchini Afrika ya Kusini siku chache zijazo itakuwa ni sehemu ya maandalizi kwa Stars, kwa mujibu wa Nooij, ambaye anasema Stars itahitajika kutoa ushindani mkubwa.

Image caption kikosi cha Taifa stars

Taifa Stars itakuwa na kibarua kigumu katika kugombea nafasi mbili kwa ajili kwenda kucheza fainali.

Stars imeshuka katika viwango vya FIFA vya mwezi April vilivyotolewa Alhamis kutoka nafasi ya 100 mpaka nafasi ya 107 na kushuka huko kuna maanisha Nooij atalazimika kufanya kazi ya ziada kupenya katika tundu la sindano.

Licha ya kushuka nafasi nne katika viwango vya FIFA, Nigeria, sasa ikiwa nafasi ya 45 ni miongoni mwa timu ngumu barani Afrika zikiwa na historia ya kufuzu kucheza kombe la Mataifa ya Afrika na hata la Dunia, sambamba na Misri, ambayo imepanda nafasi 7 katika viwango hivyo na kuwa nafasi ya 51.

Katika kundi hilo, Chad ndiyo timu iliyo chini katika viwango hivyo, ikishuka nafasi 3 na kuwa nafasi ya 151