Kusuka au kunyoa Twiga au Shepolopolo?

Image caption Shepolopolo

Ni kusuka au kunyoa ambapo kitendawili cha timu gani itafuzu kucheza fainali za michezo ya Afrika kwa upande wa soka la wanawake kati ya wenyeji Twiga Stars au Shepolopolo ya Zambia kitatenguliwa pale timu hizo zitakapokwaana katika mechi ya kufuzu Ijumaa jijini Dar es Salaam.

Kuelekea katika mchezo huo, makocha wa timu zote wametambiana huku kocha mwenyeji, Rogasian Kaijage wa Twiga Stars akijivunia kuwa uwanja wa nyumbani ambapo robo tatu ya mashabiki watakuwa upande wake.

Kaijage na nahodha wake Sophia Mwasikili wamewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuja kuwashangilia.

Kocha wa Shepolopolo, Albert Kachinga, akiwa nyuma ya magoli 2-4 katika mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Lusaka, amesema amefanyia kazi makosa yaliyosababishwa kufungwa na wana matumaini ya kushinda.

Zambia pia ina nafasi endapo itaifunga Stars kwa zaidi ya idadi ya magoli yale ya awali waliofungwa nchini mwao.

Mechi inatarajiwa kuanza majira ya saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, na tiketi za mchezo zitauzwa saa chache kabla ya mechi eneo la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku viingilio vya mchezo huo vikiwa ni shilingi za Kitanzania 5000 (wastani wa dola3 za kimarekani) kwa viti maalumu na shilingi 2000 (dola 1) kwa majukwaa yaliyobakia.

Image caption Twiga Stars

Twiga Stars ambayo katika mchezo wa awali iliibuka na ushindi wa mabao 4-2, inahitaji sare ya aina yoyote ili kuweza kufuzu kwa fainali za Michezo ya Afrika zitakazofanyika nchini Congo-Brazzavile mwezi Septemba.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, ameitakia kila la kheri timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa ajili ya timu.