Watford yaelekea kufuzu kwa Ligi Kuu

Image caption Odion Ighalo

Mshambulizi wa Nigeria Odion Ighalo, amefananisha mechi mbili za Watford zilizosalia za ligi daraha ya pili na fainali, huku klabu hiyo ikikaribia kufuzu kwa ligi kuu ya Premier nchini Uingereza.

Watford inaongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa alama moja, huku ikiwa imesalia na mechi moja ya ugenini dhidi ya Brighton na nyingine dhidi ya Sheffield Wednesday katika uwanja wao wa nyumbani.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, amesema wameafikia matokeo hayo kwa sababu ya nia, ila amesisitiza kuwa ni sharti washinde mechi hizo zilizosalia. ''Tayari tunayo tikiti ya kupandishwa daraja na kamwe hatuwezi kupoteza nafasi ya kuandikisha historia'' Alisema Ighalo.

Ushindi wao wa bao moja kwa bila dhidi ya Birmingham siku ya Jumamosi ilifufua matumaini ya Watford, na kuweka katika nafasi nzuri kuliko Bournemouth, ambayo inashikilia nafasi ya pili sawa na Middlesbrough lakini inadumishwa na idadi ya magoli.

Msimu wa mwaka wa 2012/13, Watford ilipoteza nafasi ya kupanda daraja baada ya kushindwa na Cyrstal Palace katika hatua ya muondoano.