Michuano ya Ufukweni kanda ya 5 yatajwa

Image caption wachezaji wa mpira wa wavu wakichuani pwani

Makundi kwa jili ya kufuzu kucheza michezo ya Afrika (All Africa Games) ya mpira wa wavu ya ufukweni kwa wanawake kwa nchi za Afrika kanda ya 5 yametajwa ambapo wenyeji Kenya imewekwa kundi A ikiwa na Misri, Burundi na Sudan.

Kundi B lina timu kutoka Tanzania , Uganda na Rwanda. Michuano hiyo itafanyika pwani ya Mombasa, nchini Kenya kuanzia May 7-9 ambapo washindi wawili wataungana na washindi wawili kutoka kila kanda kwa ajili ya fainali ya Michezo hiyo ya Afrika itakayofanyika nchini Congo Brazzaville kuanzia Septemba 4-19 mwaka huu.

Makamu wa raisi wa Chama cha Volleyball nchini Tanzania (TAVA), Muharrami Mchume amesema wanategemea kuwa miongoni mwa timu zitakazofuzu kucheza michezo hiyo ya Afrika ambapo timu teule ya Tanzania itaanza mazoezi mkoa wa Tanga, Kaskazini mwa Tanzania siku chache zijazo.

Shirikisho la mchezo huo barani Afrika (CAVB) hivi karibuni lilitaja kanda 7 za Afrika zitakazoshindana ili kutoa timu mbili kila kanda kwa ajili ya michezo hiyo mikubwa barani Afrika, ambapo zaidi ya wana mihcezo 3,000 watashindana katika michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, kuogelea na kukimbia (athletics).