Tutakula sahani moja na Azam -Simba.

Image caption Kocha wa Simba Sports Club,Goran Kopunovic

Wakati wapinzani wao wa jadi, Yanga wakitwaa ubingwa wa Tanzania bara baada ya kuutema msimu uliopita, mahasimu wao Simba wamesema sasa wanakula sahani moja na klabu ya matajiri ya Azam ya kugombania nafasi ya pili ili kushiriki michuano ya kimataifa

Simba imekuwa nje ya michuano ya vilabu ya CAF kwa zaidi ya miaka miwili ya kuusotea ubingwa.

Tayari Yanga imekata mzizi wa fitina na kuwa bingwa wa msimu huu wa 2014/2015 kwa kutwaa ubingwa baada ya kuwafunga Polisi Morogoro 4-1 na kufikisha pointi 55, ambazo si Simba wala Azam au timu yoyote inayoweza kuzifikia wakati ligi ikielekea ukingoni. Yanga bado ina mechi mbili mkononi.

Image caption Timu ya soka ya Azam

Azam ni ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 45 na ikiwa na mechi tatu mkononi ikiwemo ile ya kukata na shoka dhidi ya Simba ambayo huenda ikatoa picha ya mshindi wa pili. Simba, imebakiwa na mechi mbili mkononi ikiwa na pointi 41 na inahitaji kufanya kazi ya ziada kuipiku Azam.

“Tutapigana kufa na kupona ili nafasi ya pili iwe yetu tushiriki michuano ya kimataifa”, amesema kocha wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic.

Hata hiyvo, Simba inahitaji kucheza kufa na kupona kwani Azam, baada ya kuukosa ubingwa, imehamishia nguvu zake katika nafasi ya pili ili waweze kukwea pipa mwakani kimataifa. Simba imekuwa mabingwa wa Tanzania bara mara 18, Yanga wakiongoza kwa kushinda mara 25.