Yanga ni bingwa Tanzania Bara

Image caption Mashabiki wa Yanga wakifurahia ushindi

Klabu ya Yanga nchini Tanzania imekata mzizi wa fitina baada ya kunyakua ubingwa wa ligi kuu kwa msimu wa mwaka 2014/2015. Ushindi ulioupata wa magoli 4-1 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ndio ulihitimisha safari ya Yanga na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la klabu bingwa barani Afrika.

Kwa sasa Yanga, ambao wamewavua Azam ubingwa huo, ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya CAF, wakiwa na kazi ya kuitoa Etoile du Sahel mapema mwezi ujao katika hatua ya 16 ya kombe la Shirikisho.

“Nimefurahishwa na kushinda taji la ligi kuu Tanzania, wachezaji wamejituma na wamefanikiwa”, amesema kocha mkuu wa Yanga, Hans Pluijm.

Amisi Tambwe kutoka Burundi, ambaye ndiye mfungaji bora wa msimu uliopita akiwa mchezaji wa Simba, alifunga hat-trick (magoli matatu) dhidi ya Polisi Morogoro huku Simon Msuva akitupia moja.

Sherehe za kutwaa ubingwa huo ziliendelea hadi nje ya mitaa kadhaa ya Dar es Salaam kutokana na furaha ya mashabiki. Hata hivyo, Yanga haikukabidhiwa kombe kutokana na kuendelea kwa ligi.