Tanzania kujifua kanda ya 5

Image caption Wachezaji mpira wa wavu ufukweni ,wakiwa mazoezini

Tanzania imeteua wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa wavu wa ufukweni ambao wataanza mazoezi Jumatano wiki hii mkoani Tanga, Kaskazini mwa Tanzania kwa ajili ya kushiriki michuano ya kufuzu ya Kanda ya 5 kwa wanawake Afrika.

Michuano hiyo ya kufuzu ni kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kushiriki michezo ya Afrika (All Africa Games) itakayofanyika nchini Congo Brazzaville kuanzia Septemba 4 mpaka 19 mwaka huu.

Makamu wa raisi wa shirikisho la mchezo huo nchini Tanzania (TAVA), Muharrami Mchume amewataja wachezaji hao kuwa Hellen Richard, Evelyine Albert, wakitoka klabu ya Magereza na Lilian Agapa.

Mchezo wa wavu wa ufukweni unahusisha wachezaji wawili kwa kila timu.

Michuano hiyo itafanyika pwani ya Mombasa, Kenya katika beach ya Jacaranda.

Tanzania imepangwa kundi moja na Uganda na Rwanda, huku wenyeji Kenya wakiwa kundi moja na timu za Misri na Burundi.