Michuano ya gofu Burundi yaahirishwa

Wachezaji wa gofu wa kulipwa wa Tanzania wamejitoa kushiriki michuano ya wachezaji wa kulipwa ya Burundi kutokana na maandamano ya kisiasa yanayoendelea.

Hassan Kadio, Jimmy Mollel na Nuru Mollel ni miongoni mwa wachezaji wa kulipwa wa Tanzania waliokuwa wanategemewa kushiriki.

Habari kutoka kwa wachezaji hao zinasema wasingeweza kusafiri kutokana na vurugu hizo. Hata hivyo, habari zizizo rasmi zinasema michuano hiyo iliyokuwa ifanyike Jumatano, imehairishwa mpaka tarehe isiyojulikana.

Michuano hiyo hufanyika kila mwaka huku waandaaji, chama cha mchezo huo cha Burundi kikituma mialiko kwa wachezaji wa nchi mbalimbali.

Vurugu hizo, kwa mujibu wa vyombo vya habari, zinatokana na jaribio la Raisi wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza kuonesha nia ya kutaka kuongoza tena nchi hiyo kwa muhula mwingine kinyume na katiba.