Yanga yaifuata Etoile du Sahel Tunisia

Image caption Watoto wa Jangwani

Klabu ya Yanga ya Tanzania imeondoka Dar es Salaam kwa ndege ya kukodi ya serikali kuelekea Tunisia kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya raundi ya 16 bora ya Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya timu mwenyeji, Etoile du Sahel itakayochezwa hapo Jumamosi.

Wachezaji hao, wakiwa na kocha wao Hans Pluijm, wameondoka wakiwa na bashasha tele usoni baada ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya 25 ndani ya miaka 50 tangu ilipoanzishwa mwaka 1935.

Ubingwa huo ndio unampa jeuri kocha Pluijm ya kwamba wachezaji wake wako vizuri kisaikolojia kwa ajili ya kuwatoa mabingwa hao wa zamani wa kombe hilo.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam wiki mbil zilizopita, Yanga walilazimishwa sare ya 1-1 na Etoile du Sahel na sare hiyo ndio imewaweka pabaya vijana wa jangwani katika mechi yao ya Jumamosi.

Image caption Timu ya Etoile du Sahel

Etoile du Sahel, kwa upande wao, wanahitaji sare tu ya aina yoyote ile wasonge mbele huku wakijivunia kuwa uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wao.

Yanga, kwa upande mwingine, wanahitaji ushindi ili wasonge mbele na tayari tetesi kutoka Tunisia zinasema wapinzani wao wamejipanga kuhakikisha kuwa Yanga hawatoki nyumbani kwao.

Hata hivyo, kocha wa Yanga, Pluijm amesema chochote kinaweza kutokea na Yanga ikafanya maajabu dhidi ya wapinzani wao wenye rekodi kubwa na uzoefu katika michuano ya CAF.