Timu ya mpira wa pete kujifua Zanzibar

Image caption Wacheza mpira wa pete wakichuana

Timu ya taifa ya mpira wa pete ya Tanzania itaweka kambi visiwani Zanzibar ili kujiandaa na michuano ya Afrika itakayofanyika nchini Namibia tarehe 28 mwezi ujao.

Kiongozi wa chama cha mchezo huo Tanzania Bara (Chaneta), Anna Kibira amesema kuwa watachagua timu kwa kushirikiana na wenzao wa Zanzibar (Chaneza) kwa ajili ya kuanza kambi hapo Mei 17 visiwani Zanzibar.

Tanzania iliombwa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo kabla ya kuhamishiwa Namibia, lakini imeshindwa kutokana na uhaba wa fedha.

Awali, Zambia iliteuliwa kuwa mweyeji kabla ya Tanzania kuombwa na ilishindwa kwa sababu kama hizo.

Tanzania ilishindwa kushiriki michuano hiyo ya mwaka 2013 iliyofanyila Blantyre, Malawi kutokana na ukosefu wa fedha , lakini Kibira amesema watafanya jitihada ili kuhakikisha wanasafiri kwenda Namibia kushiriki.

Nchi mbalimbali za Afrika kama vile Kenya, Uganda zinategemewa kushiriki michuano hiyo.