Yanga yajifua kimataifa zaidi

Image caption Watoto wa Jangwani,Yanga.

Baada ya kupata tiketi ya kucheza katika michuano ya Kombe la Washindi barani Afrika hapo mwakani, mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga wapo katika mikakati ya kuboresha kikosi chao ili kufanye vema kimataifa.

Tayari kuna habari kuwa Yanga, waliotolewa katika kombe la Washindi barani Afrika na timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia hivi karibuni, wapo katika harakati za kutafuta mshambuliaji ili kuongeza nguvu katika safu ya mbele.

Tetesi zinasema kuwa huenda kiungo mshambuliaji, Mbrazil Andrey Countinho akaachwa na mabingwa hao licha ya kuwa na kiwango kizuri ili apatikane straika mahiri mwenye uwezo mkubwa na nguvu.

Klabu za Tanzania zimekuwa zikitolewa katika hatua za awali za michuano ya kimataifa kutokana na ukosefu wa uzoefu wa kutosha na kukosekana kwa washambuliaji mahiri.

Timu hizo zimekuwa katika harakati za kusajili wachezaji wazuri ili kujiandaa. Azam, waliokuwa wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Washindi barani Afrika, inasemekana pia wapo katika mbio za kuongeza nguvu kikosi chao, wakijiandaa na kombe la Shirikisho mwakani, baada ya kushinda nafasi ya pili katika ligi kuu iliyoisha hivi karibuni.