Steve McClaren kocha wa Newcastle United

Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England Steve McClaren, ameteuliwa kuwa Kocha mkuu wa klabu ya soka ya Newcastle United akiziba pengo la aliyekuwa kocha wa timu hiyo John Carver ambaye ametimuliwa hivi karibuni.

Kocha huyo pia ametajwa kuwepo katika bodi ya timu hiyo, huku Mike Ashley akiiacha nafasi yake katika bodi na kubaki kuwa mmiliki tu. McClaren ambaye amesain mkataba wa miaka mitatu ambao unaweza kurefushwa mpaka miaka nane, amesema kuwa anatambua wajibu wake ni kuwapa mashabiki na wapenzi wa Newcastle timu ambayo watajivunia. Steven McClaren aliiongoza England mwaka 2006 mpaka 2007, lakini pia amewahi kuzifundisha Middlesbrough, Nottingham Forest pamoja na Wolfsburg ya Ujerumani.