Tanzania kuivaa Misri michuano ya AFCON

Image caption Taifa Stars ya Tanzania ikijifua tayari kwa kuikabili Misri

Baada ya mazoezi ya wiki moja nchini Ethiopia, timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaondoka Ijumaa jioni mjini Addis Ababa kuelekea nchini Misri tayari kwa mchezo wa kwanza wa kugombea kucheza fainali za AFCON za mwaka 2017 utakaochezwa siku ya jumapili. Mechi ya marudiano itachezwa Dar es Salaam, Tanzania baada ya wiki mbili.

Kocha mkuu wa Taifa Stars Mart Nooij amesema, anashukuru maendeleo ya kambi ni mazuri na ana imani Stars itaweka kuwafunga mabingwa mara saba wa AFCON, Misri nyumbani kwao.

Stars ina kibarua kigumu dhidi ya moja ya timu bora za Afrika, Misri iliyo nafasi ya 55 katika viwango vya FIFA, wakati Stars inashika nafasi ya 127.

Nooij amesema amekuwa akiwafundisha wachezaji wake kucheza mpira wa kasi na pasi za haraka haraka, jambo ambalo wachezaji wameonyesha kufuata vizuri maelekezo yake na kusema wanamuelewa vizuri.

Akiongelea mchezo dhidi ya Misri siku ya jumapili, Nooij amesema timu inakwenda kupambana kusaka matokeo mazuri katika mchezo, nafahamu tunaenda kucheza ugenini, nimewaelekeza vijana wangu wanaocheza nafasi ya ushambuliaji kutumia vizuri nafasi tutakazozipata katika mchezo huo.

Aidha kocha Nooij amesema katika mpira hakuna kinachoshindikana, kambi ya wiki moja Addis Ababa imewasaidia wachezaji kukaa pamoja na kushika maelekezo yake vizuri, hivyo anaamini timu yake itafanya vizuri katika mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON.

Katika kikosi cha wachezaji wa 22 waliopo kambini jijini Addis Ababa hakuna mchezaji majeruhi, wachezaji wote wako vizuri kiafya, kifikra na morali ni ya hali ya juu kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya Mapharao.

Taifa Stars itaondoka Ethiopia kuelekea nchini Misri kwa shirika la ndege la Ethiopia majira ya saa 5 usiku na kufika Cairo majira ya saa 8 usiku, kisha kuunganisha safari ya kuelekea jijini Alexandria ambapo timu mchezo huo utakapofanyika.

Mchezo kati ya Misri dhidi ya Tanzania utachezwa katika uwanja wa Borg El Arab kuanzia majira ya saa 1 jioni kwa saaa za huku, sawa na saa 2 kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Waamuzi wa mchezo huo wanatokea nchini Ethiopia ambapo ni Bamlak Tessema Weyesa (mwamuzi wa kati), Kinfe Yilma (mwamuzi msaidizi wa kwanza), na Wolday Hailerague (mwamuzi msaidizi wa pili).