Azam yajifua kimataifa na kitaifa

Image caption Mabingwa watetezi wa kombe la Kagame,El Merreikh ya Sudan

Wawakilishi wa Tanzania katika kombe la Shirikisho, Azam FC wamesema watatumia michuano ijayo ya Kagame Cup kujiweka sawa kwa ajili ya ligi kuu Tanzania Bara na Michuano ya kimataifa.

Azam, baada ya kuwapokea wataalamu wake kutoka Ulaya akiwemo kocha msaidizi na meneja wa timu, imesema ikiwa chini ya kocha aliyerudi klabuni hapo, Muingereza Stewart Hall, inategemea kufanya vizuri michuano ya nyumbani na ya kimataifa.

Kocha Hall amesema anaandaa program nzuri ya mazoezi ili timu ifanye vizuri msimu ujao.Azam ilitolewa na El Merreikh ya Sudan katika hatua ya kwanza ya ligi ya mabingwa Afrika na ilipoteza ubingwa wake kwa klabu ya Yanga na kumaliza nafasi ya pili katika msimu

Tanzania imekubali kuwa wenyeji wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ngazi ya vilabu inayojulikana kama Kagame Cup.

Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ndio wamiliki wa mashindano haya na hutoa mialiko kwa vilabu vyenye sifa ya kushiriki. Watatoa orodha ya vilabu shiriki na ratiba ya michuano hiyo baade mwezi huu au mapema mwezi ujao.

Michuano hii inatarajiwa kufanyika nchini Tanzania kuanzia tarehe 11 Julai mpaka 02 Agosti 2015.

Michuano hiyo inadhaminiwa na Raisi wa Rwanda, Paul Kagame na hufanyika kila mwaka katika nchi mwanachama za ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati. Rwanda ndio ilikuwa mwenyeji wa michuano ya mwaka jana inayohusisha vilabu.