Camara:mechi dhidi ya Uganda ni muhimu

Image caption Lansana Camara(asiye na jezi-wa pili kulia) akiwa mazoezini.

Kiungo Lansana Camara kutoka Sierra Leone amesema atatumia mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya Sports Club Villa ya Uganda kuonesha uwezo wake.

Camara kwa sasa yupo katika majaribio na timu ya Yanga kwa ajili ya kusajiliwa kwa msimu ujao wa ligi kuu Tanzania Bara.

Uongozi wa benchi la ufundi wa timu hiyo, chini ya kocha Mholanzi, Hans Pluijm umempa muda zaidi kiungo huyo mwenye umbo la kiuchezaji ili aonyeshe uwezo wake na kuushawishi uongozi kumsajili.

Camara amenukuliwa akisema kuwa mechi hiyo itakuwa muhimu kwake kuonesha uwezo wake uwanjani.

"Tangu nimefika nimekuwa nikifanya mazoezi ya viungo, sasa mechi itatoa nafasi zaidi kuushawishi uongozi", amesema Camara.

Camara, ambaye alikuwa akicheza klabu ya Umea FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Sweden, alikutana na kocha mkuu wa Yanga, Hans Pluijm na kufanya naye mazungumzo kuelekea ndoto yake ya kutua katika klabu hiyo.

“ Nina furahia mazoezi yangu na mashabiki wengi wanakuja kutuangalia, hii inatia moyo”, amesema Camara, ambaye anafanya mazoezi na timu hiyo kwa sasa.

Yanga imeanza mazoezi takriban wiki mbili zilizopita katika viwanja vya kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi kuu.

Mechi hiyo inategemewa kuchezwa wikiendi ijayo.