Nyambui awa kocha wa riadha - Brunei

Image caption Nyambui akiongea na wakimbiaji

Mshindi wa zamani wa medali ya fedha ya michuano ya Olimpiki, Suleiman Nyambui amepata kazi ya kuwa kocha mkuu wa Brunei.

Nyambui, aliyeshinda medali ya Olimpiki mwaka 1980 wakati wa michuano ya Olimpiki ya majira ya joto nchini Moscow,amesema kuwa amepewa mkataba wa kuifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo kwa miaka miwili, ila atafanya kazi kwa miezi sita kuangalia mazingira.

“Wameniomba kuwa kocha kwa miaka miwili, nami nimewaomba, kwa kuanzania, kufundisha kwa miezi sita ili nione mazingira, baada ya hapo huenda nikabaki”, alisema Nyambui.

Nyambui, ambaye amesema atajiuzulu nafasi yake ya ukatibu mkuu wa chama cha Riadha Tanzania (AT), aliwahi katika miaka ya nyuma kuwa kocha nchini Marekani, visiwa vya Bahrain na alipata kufundisha nchini Australia mara kadhaa kwa mikataba ya muda mfupi mfupi.

Nyambui amesema anategemewa kuondoka Dar es Salaam kuelekea Brunei kuanza majukumu mapya.