Tanzania yampiga kalamu kocha wake

Image caption Nooij

Mkufunzi Mart Nooij amepigwa kalamu kama kocha wa timu ya taifa ya soka nchini Tanzania baada ya timu hiyo kushindwa 3-0 na Uganda nyumbani katika mechi ya awamu ya kwanza ya kufuzu kwa michuano ya CHAN.

Mechi hiyo ikiwa ni kati ya mechi tatu za Afrika mashariki wikiendi hii kwa wachezaji wanaochezea soka yao Afrika ilitawaliwa na Uganda ambao waliishinda Tanzania katika mechi za kufuzu kwa michuano hiyo msimu uliopita.

Erisa Ssekisambu alifunga katika kila kipindi kabla ya Farouk Miya kufunga kwa njia ya penalti kunako dakika za lala salama na hivyobasi kutoa ishara za kufutwa kazi kwa kocha huyo.

Nooij ameandikisha msururu wa matokeo mabaya tangu alipochukua ukufunzi wa timu hiyo miezi 14 iliopita.

Image caption Taifa Stars

Wikiendi iliopita ,Tanzania ilipoteza 3-0 kwa Misri katika mechi za kufuzu kwa kombe la Afrika mwaka 2017.

Shirikisho la soka nchini Tanzania limetangaza habari hizo na kuongezea kwamba litamuajiri mrithi wake hivi karibuni.