Vilabu ruksa kusajili 7 wa kigeni

Image caption Wachezaji ndugu kutoka Ivory Coast, Kipre na Bolou wanaochezea Azam FC ya Tanzania Bara.

Sasa ni wazi ligi kuu ya Tanzania Bara ushindani utaongezeka na kufungua milango zaidi kwa wachezaji wa kigeni baada ya vilabu kuruhusiwa kusajili wachezaji 7 wa kigeni kuanzia msimu ujao ujao wa ligi.

Awali, baadhi ya vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara vilipendekeza usajili wa wachezaji 10 wa kigeni lakini Shirikisho la mpira wa miguu (TFF) limeamua ni 7 tu wanaweza kusajiliwa na kucheza kwa wakati wote.

Katika misimu iliyopita, kila timu iliruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi watano.

Hata hivyo, si vilabu vyote vitaweza kusajili wachezaji wa kigeni kwa kuwa na vyanzo vidogo vya pesa, bali vilabu vikubwa kama vile Simba,Yanga na Azam vitaweza kumudu gharama za usajili

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, mikakati ya kusajiliwa wachezaji hawa ni haya yafuatayo:

- Mchezaji awe ni mchezaji wa timu za Taifa za nchi yake kuanzia timu ya taifa au timu za vijana za U23, U20, U19 na U17.

- Mchezaji awe anacheza katika ligi kuu ya nchi yake au nchi nyingine wakati anasajiliwa.

Wimbi la wachezaji wa kigeni linaongezeka nchini Tanzania baada ya ligi ya nchi hiyo kuwa ni ligi yenye ushindani na vilabu kutoa pesa nyingi kwa ajili ya usajili na mshahara.

Kwa habari zisizo rasmi, ligi ya Tanzania Bara inasemekana ndio ligi inayoongoza katika ukanda wa Afrika ya Mashariki kwa ushindani.