Wachezaji wa kimataifa wa Yanga waanza mazoezi

Image caption Mwenye mpira ndiye Amisi Tambwe

Mazoezi ya klabu ya Yanga yamezidi kunoga baada ya wachezaji wake wa kimataifa kuwasili ili kujiunga na timu kujiandaa na michuano ya kitaifa na kimataifa.

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amesema sasa mambo yanakwenda sawa na timu inajiweka vizuri kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na michuano ya Kombe la Kagame itakayochezwa Dar es Salaam mwezi ujao.

Wachezaji wa kimataifa wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe na Wanyarwanda Haruna Niyonzima pamoja na Mbuyu Twite wamewasili na kuongeza idadi ya wachezaji wanaondelea na mazoezi katika viwanja vya kumbukumbu ya Karume.

Wachezaji wa Yanga waliokuwa katika timu ya taifa ya Tanzania iliyofungwa 3-0 na Uganda katika mechi ya awali ya kufuzu kucheza michuano ya CHAN nao wanategemewa kujiunga na timu baada ya kuwasili kutoka Zanzibar na kuifanya Yanga kuwa kamili kimaandalizi.

Kwa sasa Yanga ina wachezaji watano wa kimataifa ambao ni Tambwe, Twite, Niyonzima, Kpah Sherman na Mbrazil Andrey Coutinho, ambao pia wameanza mazoezi baada ya mapumziko ya ligi..