Taifa Stars yapata kocha mpya

Image caption Kocha mpya wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania - TFF, Jamal Malinzi leo ameagana rasmi na aliyekua kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania mholanzi Mart Nooij na kumtangaza Charles Boniface Mkwasa kuwa kocha mpya wa timu ya Taifa ya Tanzania akisaidiwa na Hemed Moroco

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi amesema kwamba, kocha mpya wa timu ya taifa, Charles Boniface Mkwasa atakuwa analipwa sawa na kocha Mholanzi, Mart Nooij aliyeondolewa.

Nooij aliyekuwa analipwa dola za Kimarekani 12,500 (zaidi ya Sh. Milioni 25) kwa mwezi, alifukuzwa mwishoni mwa wiki baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Mkwasa ambaye ni Kocha Msaidizi wa Yanga na Morocco kocha wa Mafunzo watafanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo timu ya taifa itakua na michezo ya kuwania kufuzu kwa CHAN na AFCON.

Malinzi amesema uteuzi wa makocha hao wazawa umezingatia vigezo vya makocha wa timu ya Taifa kuwa na leseni A ya ukocha kutoka CAF au zinazofanana kutoka mashiriksho mengine duniani wanaozifanyia kazi, jambo ambalo makocha hao wazawa wamekizi.

Aidha Kamati ya utendaji ya TFF Iimemteua Alhaj Ahmed Mgoyi kuwa mratibu wa timu ya Taifa, lengo la uteuzi huo wa Mgoyi ni kuwa kiunganishi kati ya kamati ya Utendaji na timu ya Taifa.