Azam kusajili wapya

Image caption Azam wakishangilia

Baada ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kucheza ligi kuu kutoka watano (5) hadi 7, klabu ya Azam ina mipango ya kusajili wachezaji kutoka nchi za Zambia, Ivory Coast na Rwanda.

Tayari klabu hiyo ina wachezaji wa kimataifa wakiwemo wa Ivory Coast ndugu wawili, Kipre na Bolou na beki mwenye nguvu, Pascal Wawa.

“kuna mshambuliaji kutoka Zambia, kuna golikipa toka Ivory Coast, kuna kiungo toka Rwanda na wengine kadhaa ambao wapo kwenye mipango yetu”, amenukuliwa kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall katika website ya klabu hiyo tajiri.

“Nafasi ni mbili,kabla ya kuamua yupi atakuja nahitaji kufanya tathmini ya kina kuangalia ni eneo gani lina mapungufu kasha tuweze kuamua” alisema Stewart Hall, kocha mwenye uzoefu wa kutosha na ligi kuu ya Tanzania.

Kikosi cha Azam FC kinachojiandaa na mashindano ya Kagame Cup kinaendelea na maandalizi yake kwenye viunga vya Azam Complex huku benchi jipya la ufundi likifurahia vipaji vilivyopo.

Wasaidizi wa kocha Muingereza Stewart Hall waliotoka Uingereza na Romania wameonekana kufurahishwa sana na nidhamu, vipaji na kujituma kwa wachezaji waliowakuta Azam FC.

Kwa mujibu wa mtandao wa klabu ya Azam FC, benchi la ufundi la timu hiyo itakayoiwakilisha nchi katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika wanatumia maarifa yao yote kuhakikisha wanaifanya Azam FC klabu inayoheshimika Afrika.

Wachezaji wa kigeni wameongezea utamu wa mazoezi hayo ambayo wiki iliyopita yalitawaliwa na wachezaji wa kikosi cha vijana (Under 20)

Azam FC imekuwa ikifanya mazoezi ya kujenga mwili zaidi kwa kukimbia, Gym, Kuogelea na kuchezea mpira.