Copa America:Paraguay yaiondoa Brazil

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Copa America:Paraguay yaiondoa Brazil

Paraguay imejikatia tikiti ya nusu fainali ya mchuano wa Copa America baada ya kuilaza Brazil katika hatua ya robo fainali.

Paraguay ilijikatia tikiti hiyo baada ya kuilaza Brazil mabao 4-3 kwa mikwaju ya penalti.

Timu hizo zilikuwa zimetoka sare ya 1-1 katika muda wa kawaida.

Paraguay sasa itakabiliana na Argentina katika nusu fainali.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Robinho alikuwa ameiweka Brazil kifua mbele kunako dakika ya 15

Robinho alikuwa ameiweka Brazil kifua mbele kunako dakika ya 15 ya kipindi cha kwanza baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Dani Alves .

Hata hivyo Thiago Silva aliadhibiwa kwa kuunawa mpira ndani ya eneo la lango na Derlis Gonzalez hakufanya masihara mbele ya lango.

Alifuma mkwaju kimiani na kupelekea mechi hiyo kuwa sare ya 1-1.

Ilipofika wakati wa mikwaju ya penalti Brazil walipoteza nafasi mbili na hivyo Gonzalez akaihakikishia Paraguay fursa ya kuchuana na Argentina katika nusu fainali ya kombe hilo.

Argentina walikuwa wameshajikatia tikiti ya nusu fainali baada ya kuitamausha Colombia katika ile robo fainali ya kwanza.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Paraguay watachuana na Argentina julai mosi katika uwanja wa Concepcion.

Paraguay watakuwa wanatafuta taji hilo la Copa America waliloshinda mara ya mwisho mwaka wa 1979.

Watachuana na Argentina julai mosi katika uwanja wa Concepcion.

Chile kwa upande wake itakuwa inatarajia mashabiki wake wataisaidia kuizima Peru katika ile nusu fainali nyengine itakayoandaliwa Santiago.