FIFA yampiga marufuku afisa kwa miaka 7

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption FIFA yampiga marufuku afisa kwa miaka 7

Afisa wa shirikisho la soka duniani ,FIFA aliyesimamia jopo la kutathmini uwenyeji wa kombe la dunia la mwaka wa 2018 na 2022 amepigwa marufuku ya miaka 7

FIFA imetangaza kuwa bwana Harold Mayne-Nicholls, 54 hataruhusiwa kushiriki maswala yeyote yanayohusiana na kandanda kwa kipindi cha miaka 7 ijayo.

Kamati ya maadili ya FIFA imesema kuwa itatangaza wazi madai dhidi yake pindi marufuku hiyo itakapoaanza kutekelezwa.

Haki miliki ya picha FIFA
Image caption Mayne-Nicholls anahoji kwanini kauli hiyo imechukuliwa na kutangazwa wakati ambao FIFA inafahamu fika kuwa anaendelea kukata rufaa

Bwana Mayne-Nicholls anapanga kukata rufaa ya madai dhidi yake.

Aidha bwana Mayne-Nicholls anahoji kwanini kauli hiyo imechukuliwa na kutangazwa wakati ambao FIFA inafahamu fika kuwa anaendelea kukata rufaa.

Mayne-Nicholls aliyekuwa wakati mmoja mwenyekiti wa shirikisho la soka la Chile alitajwa miongoni mwa watu 5 ambao kamati ya maadili ya FIFA ilkuwa imeanzisha uchunguzi.

Alikiri wakati wa uchunguzi kufanya mazungumzo ya kibinafsi na wakuu wa shirikisho la soka la Qatar akitaka jamaa wake waajiriwe katika chuo cha mafunzo ya kisoka ya Aspire .

Kulingana na barua pepe zilizodukuliwa huo ulikuwa ni ushahidi tosha wa kumchukulia hatua bwana Mayne-Nicholls.

Image caption Harold Mayne-Nicholls, 54 hataruhusiwa kushiriki maswala yeyote yanayohusiana na kandanda kwa kipindi cha miaka 7 ijayo.

Mayne-Nicholls aliongoza kamati ya FIFA iliyokuwa na jukumu la kupiga msasa maombi ya uwenyeji wa fainali ya kombe la dunia mwaka wa 2018 na 2022.

Uwenyeji wa mashindano hayo ulipewa Urusi na Qatar mtawalia.

Katika ripoti yake aliyoichapisha mwaka wa 2010, bwana Mayne-Nicholls alielezea hofu kuwa haitawezekana Qatar, kuandaa kombe la dunia kwani viwango vya joto nchini humo hutimia hata nyuzi joto 50'C.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Maafisa 9 wa FIFA wanaendelea kuchunguzwa kufuatia madai ya utoaji hongo,ama utumiaji wa mamlaka yao vibaya.

Mayne-Nicholls ni miongoni mwa maafisa waliotaka ripoti kamili ya FIFA kuhusiana na uwenyeji wa kombe la dunia la mwaka wa 2018 na 2022 kuchapishwa kikamilifu na wazi.

Mwezi desemba FIFA iliamua kuchapisha ''nakala halali kisheria'' iliyoandikwa na Mwanasheria kutoka Marekani Michael Garcia.

Bwana Garcia baadaye alijiuzulu akidai kuwa shirikisho hilo halikuwa tayari kuwa wazi kuhusiana na yaliyojiri katika utoaji zabuni wa mashindano hayo mawili ya kombe la dunia.

Wakati hayo yakijiri Maafisa 9 wa FIFA wanaendelea kuchunguzwa kufuatia madai ya utoaji hongo,ama utumiaji wa mamlaka yao vibaya.