Voliboli:Kenya yashinda dhahabu Grand Prix

Image caption Kenya ndio mabingwa wa taji la voliboli katika Grand Prix

Timu ya Kenya ya voliboli ya wanawake ndio mabingwa wa mwaka huu wa mashindano ya Grand Prix.

Kenya imesajili ushindi mkubwa wa seti 3-1 dhidi ya Peru katika fainali ya mashindano ya voliboli ya wanawake ya Grand Prix kundi la tatu mjini Canberra, Australia Jumapili.

Kenya ilisajili ushindi wa alama 21-25, 25-17,25-22 na kisha 25-23.

Kufuatia ushindi huo Kenya ndiyo nchi ya kwanza ya Afrika kushinda taji la Grand Prix, ushindi ambao sasa umewapandisha kidada hao Malkia hadi kundi la pili.

Image caption Kenya imesajili ushindi mkubwa wa seti 3-1 dhidi ya Peru

Mercy Moim alikua nyota wa Kenya kwa kuipatia timu yake pointi 22 akifuatiwa na Ruth Jepngetich pointi 17 .

Kwa upande wa Peru Levvy Angela aliongoza na pointi 26.

Mamia ya Wakenya wanaoishi Australia wakiongozwa na balozi wa Kenya nchini humo Isaiah Kabira waliwashangilia warembo hao wa Kenya waliovalia mavazi ya kuvutia ya rangi nyeupe na kijani kibichi.

Image caption Mercy Moim alikua nyota wa Kenya kwa kuipatia timu yake pointi 22

Peru ilishinda seti ya kwanza 25-21 lakini katika seti ya pili Kenya ilichangamka na kuibuka mshindi 25-17 na kutoka hapo Peru, ambao wanashiriki mashindano haya ya Grand Prix kwa mara ya nne, hawakuweza tena kutetemesha kina dada wa Kenya walioshinda seti zifuatazo 25-22 na 25-23.

Huku wachezaji wa Kenya wakidondokwa na machozi ya furaha, Peru nao waliambulia kilio cha kuchapwa na mabingwa wa Afrika kwani waliingia uwanjani na matumaini makubwa ya ushindi ikikumbukwa kwamba walishinda Kenya katika raundi ya kwanza nchini Mexico.

''Huu ndio mwanzo wa matokeo mengine bora zaidi katika mashindano ya dunia,'' anasema nahodha wa Kenya Praxidis Agala

Image caption Nahodha wa Kenya Braxcedes Khadambi ameomba serikali ufadhili zaidi

''Ushindi wetu unadhihirisha wazi kwamba sio riadha tu ndio mchezo Kenya inafanya vyema.''

''Tunashukuru Wakenya wanaoishi hapa kwa kutushangilia kuanzia mwanzo hadi mwisho.''

Image caption Kenya ndio taifa la kwanza Afrika kutwaa taji hilo

Kocha wa Kenya David Lung'aho anasema:

''Tuko tayari kupambana na miamba ya dunia.''

''Tulitizama kwa makini kanda za mechi za Peru walizocheza na tukapata mbinu ya kuwabana''.

Image caption Kenya sasa inajiandaa kwa kombe la dunia litakalokuwa Japan

''Sasa tuanaangazia kombe la dunia nchini Japan na michezo ya mataifa ya Afrika nchini Congo Brazaville mwezi wa Septemba.''

Kenya ilishiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya Grand Prix mwaka jana na kumaliza nafasi ya tano katika kundi la tatu.

Image caption Wakenya wanaoishi Australia waliwashabikia Malkia

Ushindi wao dhidi ya Peru umepokewa kwa vishindo na mashabiki nchini Kenya baadhi yao kwenye mtandao wa Facebook wakimuomba Rais Uhuru Kenyatta awape siku moja ya kupumzika wakailaki timu ya Kenya.

Kulingana na mwenyekiti wa shirikisho la voliboli nchini Kenya, Waithaka Kioni, timu ya Kenya huenda ikarudi nyumbani Jumanne usiku.

Kioni ameiomba serikali itoe fedha za kuwawezesha kufanya mazoezi ng'ambo kabla wasafiri kwa kombe la dunia na michezo ya mataifa ya Afrika.