Wateuliwa kushikiri ndondi C Brazaville

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ndondi

Mabondia nyota wa Kenya Benson Gicharu uzani wa bantam, Rayton Okwiri uzani wa welter na Nick Abaka uzani wa middle wameruhusiwa na shirikisho la kimataifa la ndondi, Aiba, kuiwakilisha Kenya katika michezo ya mataifa ya Afrika mwezi Septemba nchini Congo Brazaville.

Habari hizi ni kwa mujibu wa naibu wa mwenyekiti wa chama cha ndondi cha Kenya Albert Matito.

Awali Aiba ilisema kwamba hawataruhusu mabondia hao wa Kenya washiriki michezo hiyo kwa sababu wanashiriki katika ndondi za kulipwa za Aiba.

Lakini Matito anasema mwenyekiti wa chama cha ndondi cha Kenya John Kameta amezungumza na wakuu wa Aiba wakakubaliana mabondia hao watatu washiriki michezo hiyo.

''Sote tumefurahishwa na uamuzi huo kwa sababu tunajua uwezo wa mabondia wetu na kwa vile wameshiriki ndondi za kulipwa za Aiba sasa wana mbinu mpya za kupambana na wapinzani wao huko Congo,'' alisema Matito.

Okwiri ndiye bondia pekee wa Kenya aliyeshinda medali katika michezo ya kumi ya mataifa ya Afrika iliyofanyika mwaka wa 2011 nchini Msumbiji aliporudi nyumbani na shaba.

Kenya ilimaliza ya kumi pamoja na Lesotho na Uganda huku Algeria ikiibuka mshindi na jumla ya medali saba, tatu za dhahabu. Mauritius ilimaliza ya pili na Cameroon ya tatu.