FIFA kuchagua rais mpya Februari 2016

Haki miliki ya picha PA
Image caption FIFA kuchagua rais mpya februari 2016

Shirikisho la soka duniani Fifa litaandaa kongamano la dharura kuchagua rais mpya tarehe 26 mwezi februari mwakani.

Hii ni licha ya rais aliyeko sasa Sepp Blatter kutangaza nia ya kuondoka mamlakani wiki moja tu baada ya kuchaguliwa upya kuwa rais wa shirikisho hilo tarehe 26 mwezi Mei.

Tangazo hilo lilifuatia juma lenye matukio na madai ya ulaji rushwa na ufisadi miongoni mwa maafisa wakuu wa FIFA.

Viongozi watakaokuwa na ari ya kurithi kiti hicho cha rais wa FIFA,sharti wawasilishe rasmi maombi yao kabla ya tarehe 26 mwezi Oktoba mwaka huu.

Rais wa shirikisho la soka barani Ulaya (Uefa) Michel Platini, anadaiwa kupata shinikizo kutoka kwa viongozi wengi wa bara hilo kuwasilisha ombi lake la kuwa rais wa FIFA.

FIFA inatarajiwa kuandaa mkutano na waandishi wa habari muda mchache ujao.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wagombea kiti cha Urais sharti wawasilishe rasmi maombi yao kabla ya tarehe 26 mwezi Oktoba mwaka huu.

Kufikia wakati wa uchaguzi huo mpya Blatter atakuwa tayari keshahudumu kwa miezi tisa tangu atoe tangazo la kujiuzulu kufuatia shtuma kali za ufisadi dhidi ya shirikisho na haswa maafisa wakuu wa FIFA.

Mapema hii leo mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo wa mwezi Mei, mwanamfalme kutoka Jordan Prince Ali bin al-Hussein alimtaka kiongozi huyo mswisi kunga'tuka mamlakani mara moja.

Mwanamfalme al-Hussein,alisema ''Blatter lazima ajiuzulu na aondoke mara moja''

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Prince Ali bin al-Hussein alimtaka kiongozi huyo mswisi kunga'tuka mamlakani mara moja

Haifai aendelee kuingoza FIFA.

Tume maalum iundwe na ipewe mamlaka ya kusimamia uchaguzi mkuu wa FIFA .''aliongezea Prince al-Hussein.

Mkutano huo wa leo pia unatarajia kutaja baadhi ya mambo yatakayorekebishwa ikiwa ni pamoja na kuweka kikomo cha muhula cha urais na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa shirikisho hilo.

Hatua ya kuchapisha mishahara na marupurupu ya viongozi wa juu wa shirikisho hilo pia itajadiliwa.