Michel Platini kuwania urais wa FIFA

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Sepp Blatter na Platini

Rais wa shirikisho la soka barani Ulaya UEFA Michel Platini ametangaza azma yake ya kuwania urais wa shirikisho la soka duniani FIFA.

Katika barua iliotumwa kwa rais na makatibu wakuu wa shirikisho hilo lenye wanachama 209,amesema kuwa uamuzi huo ni wa kibinafsi ambapo alipima uzani wa yeye kuliongoza shirikisho hilo pamoja na ule wa hatma yake maishani.

''Pia niliongozwa na uungwaji mkono ninaopata'', alisema bwana Platini ambaye ameongezea kwamba atafanya kazi kwa moyo wake wote kwa maslahi ya soka.Kuna wakati katika maisha ambapo ni lazima uchukue hatma yako mikononi mwako,alisema.Niko katika uamuzi muhimu sana katika maisha yangu na hatma yangu ya baadaye na matukio yanayoathiri maisha ya FIFA ya baadaye''.

Michel Platini,ambaye amekuwa rais wa UEFA tangu mwaka 2007 pamoja na kuwa mwanachama wa kamati ya shirikisho la soka duniani FIFA tangu mwaka 2002,ameongezea kuwa katika nusu ya karne iliopita FIFA imekuwa na marais wawili pekee.

Lakini matukio ya hivi karibuni yalililazimisha shirikisho hilo kufungua ukurasa mpya na kuangazia uongozi wake.