Kocha wa zamani wa Ghana afariki

Image caption Charles Kumi Gyamfi baada ya kustaafu kama kocha

Mchezaji maarufu wa kandanda wa zamani wa Ghana, aliyekuwa mchezaji wa timu ya taifa na kisha kocha, Charles Kumi Gyamfi, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 85.

Gyamfi alikuwa mchezaji wa kwanza kutoka barani Afrika kucheza soka ya kulipwa nchini Ujerumani, alipojiunga na klabu ya Fortuna Dusseldorf mwaka 1960 na pia alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ghana, Black Stars.

Image caption Charles Kumi Gyamfi akiwa wachezaji wengine wa Ghana miaka sitini

Kama kocha alishinda Kombe la taifa bingwa barani Afrika ACN, mara tatu akiwa na Ghana, mwaka 1963, 1965 na 1982.

Ufanisi huo ulimfanya kuwa kocha wa timu ya taifa aliyefanikiwa zaidi Afrika, rekodi ambayo ilidumu muda mrefu hadi ilipovunjwa na Hassan Shehata wa Misri aliyeshinda kombe lake la tatu 2010.

Shirikisho la Kandanda la Ghana, GFA lilisema kupitia kwa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa "Ni kwa huzuni nyingi ambapo tumepokea habari za kufariki kwa kocha na mchezaji soka maarufu wa Ghana C.K. Gyamfi.

"shirikisho la GFA linasikitika sana kumpoteza mwanasoka na mkufunzi mwenye kipaji adimu aliyebadilisha maisha na wachezaji wengi wa soka nchini Ghana.

"Tunaipa pole familia ya CK Gyamfi na sana sana kwa mkewe, watoto, marafiki na wapendwa."