Coleman: Wales wafaa “kutekwa na furaha”

Gareth Bale
Image caption Gareth Bale wa Wales baada yao kulaza Cyprus 1-0

Meneja wa timu ya taifa ya kandanda ya Wales Chris Coleman amewahimiza mashabiki wakubali “kutekwa na furaha ya ufanisi” lakini akasema wachezaji wake hawatafanya hivyo hadi wafuzu kwa Euro 2016.

Baada ya kucharaza Cyprus 1-0 Alhamisi, Wales watafuzu wakiandikisha ushindi dhidi ya Israel Jumapili.

Coleman anaamini kufikisha kikomo kipindi cha miaka 58 cha Wales kukosa kushiriki dimba kubwa itakuwa zawadi kubwa kwa mashabiki wa timu hiyo.

“Kwa mashabiki wa Wales wanaotusubiri turejee nyumbani, sisimkeni,” Coleman amesema.

"Ujumbe wangu kwao ni kwamba wasisimke na kutekwa na furaha. Wafurahie hili kwani wamesubiri muda mrefu sana.

“Lakini sisi hatuwezi kutekwa na hilo. Siwezi, wachezaji hawawezi, na wakufunzi pia na hatutatekwa na furaha.”

Coleman ameongeza kuwa bila kujali kama yeye na wachezaji wake wamechoka kimwili na kiakili, kwa sasa lazima waangazie kujiandaa kwa mechi hiyo kubwa ya Jumapili.

"Lazima tutimize matarajio. Tumefanya hivyo kufikia sasa na twatumai kwamba tutafanya hivyo tena,” mkufunzi huyo wa umri wa miaka 45 ameongeza.

Wales kwa sasa wamo alama tatu mbele kileleni Kundi B wakiwa wamesalia na mechi tatu, na wamekaribia sana kucheza fainali za dimba kubwa tangu kushiriki kwao fainali za Kombe la Dunia 1958.

Baada ya kukaribisha Israel uwanja wa Cardiff Jumapili, vijana hao wa Coleman watakuwa na mechi mbili dhidi ya Bosnia-Herzegovina na moja dhidi ya Andorra Oktoba.

Ushindi dhidi ya Israel utatosha kuwafikisha Euro 2016, lakini Coleman anasisitiza wachezaji wake hawawezi kuthubutu kufikiria kwamba washafika Ufaransa.

"Hatuwezi kuutoroka ukweli. Ukiangalia kundi letu lilivyo, tunahitaji kushinda mechi moja tu kujihakikishia nafasi Ufaransa 2016, hilo twajua,” akasema.

"Lakini wachezaji, nakuahidi, hawataji hilo kamwe. Wanajua hilo lipo, wanajua kila mtu atakuwa akizungumzia nini nyumbani.

"Waliwaona mashabiki 4,000 waliojitokeza kuwashangilia [Alhamisi], lakini hilo halifai kutufanya tusahau lengo letu.”