FA haitamuadhibu Mourinho

Image caption Imethibitika kuwa Jose Mourinho hakuzungumza lugha chafu dhidi ya Daktari wa Chelsea,Eva Carneiro

Meneja wa klabu ya Chelsea Jose Mourinho hataadhibiwa na Chama cha Soka cha England FA,baada ya kuthibitika hakutumia lugha mbaya dhidi ya aliyekuwa daktari wa timu Eva Carneiro.

Fa ilipitia mikanda ya video iliyohusika na tukio hilo la Kocha Jose Mourinho na Eva Carneiro ambapo ilionekana kama kocha huyu alitumia lugha chafu kwa daktari huyo.

Dokta Carneiro aliingia uwanjani kumtibu mshambuliaji Eden Hazard wakati wa dakika za lala salama kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Swansea, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mara baada ya Mechi hiyo na Swansea, Dokta huyo aliondolewa kuihudumia Timu ya Kwanza ya Chelsea.

Dokta Eva Carneiro amebwaga manyanga kuwepo Chelsea licha ya kutakiwa kurudi kazini na sasa yuko mbioni kusaka Sheria katika mamlaka husika.