Nyota mwingine wa Nigeria ajitoa Super Eagles

Emenike Haki miliki ya picha AFP
Image caption Emenike amechezea timu ya taifa ya Nigeria kwa miaka mitano

Nyota mwingine wa timu ya taifa ya Nigeria Super Eagles Emmanuel Emenike ametangaza kwamba amestaafu kutoka timu hiyo ya taifa.

Emenike, 28, ametangaza hayo siku chache tu baada ya golikipa wa timu hiyo Vincent Enyeama naye pia kutangaza kwamba anastaafu.

Wachezaji hao wawili wametumia mtandao wa kijamii wa Instagram kutangaza habari hizo.

Mshambuliaji huyo amenukuliwa na gazeti la Premium Times la Nigeria akisema:

"Imekuwa furaha kuu sana kwangu kuchezea taifa hili tukufu. Zikuwahi kujutia hili na nafikiri huu ndio wakati bora zaidi wa kufikisha kikomo (uchezaji wangu).

"Nawashukuru sana mashabiki ambao wameniunga mkono muda huo wote wakati wa mema na mabaya.”

Habari ya kustaafu kwake zimepokelewa kwa hisia mseto, na kitambulisha mada #Emenike kinavuma katika mtandao wa kijamii wa Twitter nchini Nigeria.

Emenike alichezea Super Eagles mechi 35 na kuwafungia mabao 16 katika miaka mitano aliyochezea timu hiyo ya taifa.

Alikuwa mfungaji mabao bora katika fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika (Afcon) 2013.