Chelsea washindwa kutamba Ulaya

Chelsea Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mourinho alifurahishwa na na hali kwamba timu yake haijafungwa bao mechi mbili mfululizo

Chelsea walitoka sare tasa mechi yao ya tatu katika Kundi G kwenye mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ugenini dhidi ya Dynamo Kiev.

Vijana hao wa Jose Mourinho waligonga mlingoti wa goli mara mbili na pia wakanyimwa penalti.

Eden Hazard alikaribia sana kufunga, lakini kipa Oleksandr Shovkovskiy akagongesha mpira wake kwenye mlingoti.

Winga wa Dynamo Kiev Andriy Yarmolenko alishambulia sana kutoka kulia lakini aliishia kupokonywa mpira. Alipokonywa mpira mara 25 kwenye mechi hiyo.

Chelsea walifaa kupewa penalti baada ya Cesc Fabregas kuanguka alipokabiliwa vikali na Serhiy Rybalka lakini refa hakusikia kilio chao.

Frikiki ya Willian iligonga mwamba wa goli kabla ya Asmir Begovic kumzuia mchezaji mwenyeji Derlis Gonzalez kuwafunga Chelsea kwenye mechi hiyo iliyochezewa Ukraine.

Vijana hao wa Mourinho sasa wameshinda mechi moja pekee kati ya tano walizocheza majuzi zaidi katika mashindano yote.

Hata hivyo, uchezaji wao ulionekana kuimarika pakubwa Ulaya tangu walipolazwa na Porto Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2-1 ugenini Septemba 29.

Ushindi wa Porto 2-0 dhidi ya Maccabi Tel-Aviv unawafanya Chelsea kusalia nambari tatu kundini wakiwa na alama nne, moja nyuma ya Kiev na alama tatu nyuma ya viongozi wa kundi Porto.