Van Gaal: Man City wana nafasi nzuri ya kushinda debi

Louis van Gaal Haki miliki ya picha PA
Image caption Manchester City ndio wanaoongoza Ligi ya Uingereza kwa sasa

Meneja wa Manchester United Louis van Gaal amesema Manchester City ndio walio kwenye nafasi nzuri ya kushinda debi ya Jumapili, licha ya mechi hiyo kuchezewa Old Trafford.

City wameshinda sita kati ya debi nane za majuzi zaidi za Manchester, kuanzia ushindi wao wa 6-1 2011.

Van Gaal anahisi kuwa hali kwamba Blues ndio wanaoongoza Ligi ya Premia kwa sasa ina maana kwamba ndio wanaofaa kupigiwa upatu kushinda.

“Wanaongoza. Sisi tuko nambari tatu. Kuna tofauti kubwa ya mabao. Na tofauti ya alama. Wanapigiwa upatu.”

Maneno hayo ya Van Gaal yanakaribiana sana nay a mtangulizi wake David Moyes kabla ya mechi ya Old Trafford dhidi ya mahasimu wengine wakuu wa United, Liverpool.

Mtazamo wa Moyes ulichukuliwa kuwa mbaya ikizingatiwa kwamba wakati huo klabu yake ilikuwa ndio mabingwa watetezi.

Baada ya mechi hiyo, ambayo Liverpool walishinda 3-0, meneja wa Liverpool wakati huo Brendan Rodgers alisema daima hawezi akaamini wapinzani wake wana nafasi nzuri ya kushinda mechi Anfield.

Kinyume na Moyes hata hivyo, Van Gaal amefanikiwa kushinda ‘wapinzani wanne wakuu’ wa United, wakiwemo City kwenye debi ya mwaka jana.

Meneja huyo wa zamani wa Ajax, Barcelona na Bayern Munich anafahamu vyema sana umuhimu wa mechi hiyo ya wikendi hii kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Lakini licha ya uhasama wa kinyumbani kati ya City na United, Van Gaal amesisitiza kwamba hataingiza hisia kwenye mechi hiyo ndipo timu yake iwe na nafasi nzuri ya kushinda debi ya pili mfululizo Old Trafford.