Villa yamtimua Sherwood

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kibarua cha Tim Sherwood chaota nyasi

Klabu ya soka ya Aston Villa imemfukuza kazi Meneja wake Tim Sherwood baada ya kushika wadhifa huo kwa Miezi minane.

Sherwood alishuhudia timu yake ikiendelea kupoteza mchezo katika ligi kuu ya England kwa kuchapwa na Swansea kwa mabao 2-1.

Kocha wa timu ya vijana chini ya Miaka 21 wa Aston Villa, Kevin MacDonald, ndiye atakayeshika Umeneja kwa muda mpaka kupatikana kwa kocha mpya

Meneja wa zamani wa Everton na Manchester United David Moyes, ametajwa katika orodha ya makocha wanaohitajika kuchukua nafasi hiyo.

Sherwood aliteuliwa kuwa Meneja Mwezi Februari Mwaka huu kumbadili Paul Lambert na kufanikiwa kuwapeleka Villa Fainali ya FA CUP na pia kuwanusuru kushushwa Daraja toka Ligi Kuu England walipomaliza Nafasi ya 17.