Mourinho ashtakiwa utovu wa nidhamu

Mourinho Haki miliki ya picha EPA
Image caption Klabu ya Chelsea imekuwa ikiandikisha matokeo mabaya msimu huu

Jose Mourinho amefunguliwa mashtaka ya utovu wa nidhamu na Shirikisho la Soka la Uingereza kwa sababu ya lugha aliyoitumia na vitendo vyake wakati wa mechi ambayo Chelsea walichapwa na West Ham United wikendi.

Mourinho alifukuzwa eneo la marefa uwanjani baada yake kwenda kutaka kuzungumza na refa Jon Moss katika chumba chake wakati wa mapumziko mechi hiyo ya Jumamosi.

Klabu zote mbili pia zimeshtakiwa kwa kushindwa kudhibiti wachezaji na zimepewa hadi Oktoba 29 kujibu mashtaka hayo.

Chelsea tayari wanakabiliwa na faini ya £25,000 kwa wachezaji zaidi ya watano kupewa kadi za manjano wakati wa mechi hiyo ya Ligi ya Premia.

Kando na kadi mbili alizoonyeshwa Nemanja Matic, Chelsea pia walishuhudia wachezaji wao Cesar Azpilicueta, Willian, Cesc Fabregas, John Mikel Obi na Diego Costa wakilishwa kadi uwanjani Upton Park.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Matic alipewa kadi mbili za manjano

Msaidizi wa Mourinho Silvino Louro pia alifukuzwa eneo lake wakati wa mechi hiyo na vilevile ameshtakiwa kwa utovu wa nidhamu.

Klabu hiyo pia itatakiwa kueleza wasimamizi wa Ligi ya Premia ni kwa nini Mourinho alikosa kuzungumza na wanahabari baada ya mechi hiyo.

Mechi hiyo ilikuwa ya tano kwa Chelsea kushindwa katika mechi 10 za ligi msimu huu na inawaacha mabingwa hao watetezi wakiwa nambari 15 na alama 11, alama 11 nyuma ya viongozi Manchester City.