TP Mazembe 2-1 USM Alger klabu bingwa Afrika

Image caption TP Mazembe 2-1 USM Alger

TP Mazembe wameweka mkono mmoja kwenye kombe la klabu bingwa barani Afrika baada ya kushinda mkondo wa kwanza wa fainali dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Mazembe iliilaza USM Alger ya Algeria mabao 2-1 katika fainali hiyo iliyochezwa jumamosi.

Mshambuliaji wa Zambia, Rainford Kalaba na Mbwana Samatta kutoka Tanzania waliwafungia Mazembe na kuwapa ushindi muhimu ugenini.

Wenyeji wao walikosa jibu lakini wakanusurika aibu baada ya mchezaji wa akiba Mohamed Seguer kuifungia USM na kuwatuliza mashabiki wa nyumbani katika uwanja wa Stade Omar Hamadi Algiers.

Mazembe, sasa wanahitaji kutoka sare ama kuzuia wasifungwe zaidi ya bao moja watakapowapokea mahasimu hao mjini Lubumbashi wikiendi ijayo.

Mazembe walikuwa na fursa nzuri ya kuibuka na ushindi mkubwa zaidi huko Algiers ila penalti ya Nathan Sinkala ikaokolewa.

Image caption Timu hizo zitakutana tena jumapili ijayo Lubumbashi

Hata hivyo makocha wote wawili watalazimika kuimarisha nidhamu katika vikosi vyao kwani wote walimpoteza mchezaji mmoja kwa sababu ya utovu wa nidhamu.

Kalaba aloneshwa kadi nyekundu kwa kumsukuma mpinzani wake huku Hocine El Orfi akioneshwa kadi nyekundu kwa kuunawa mpira mbele ya lango.

Klabu bingwa itatuza dola milioni moja u nusu na nafasi ya kuiwakilisha Afrika katika mashindano ya kuwania ubingwa wa dunia wa vilabu huko Japan baadaye mwaka huu.