Arsenal kupimana nguvu tena na Bayern

Arsenal Haki miliki ya picha Getty
Image caption Arsenal walichapa Bayern 2-0 mechi ya mkondo wa kwanza

Difenda wa Arsenal Per Mertesacker amesema klabu ya Bayern Munich kutoka Ujerumani itataka sana kuonyesha kwamba ndiyo bora zaidi, klabu hizo mbili zitakapokutana leo katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

“Sisi tuliokuwa ndio timu ya kwanza kuwakaripia na kuwashinda,” alisema Mertesacker kuhusu ushindi wa Arsenal wa 2-0 nyumbani.

“Watataka sana kudhihirisha kwamba ndio bora kutushinda.”

Nahodha wa Bayern, Philipp Lahm amesema hawakuathirika kwa vyovyote vile na kichapo hicho kutoka kwa Arsenal.

“Tunaongoza Bundesliga na kundi letu Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya,” amesema.

“Hatukuumizwa na ushindi huo wa ugenini. Tutachezea nyumbani na ni mechi kubwa. Tunataka kushinda na kuimarisha uongozi wetu kileleni mwa kundi.”

Mafowadi wa Arsenal Theo Walcott na Alex Oxlade-Chamberlain wako nje hadi mwishoni mwa mwezi huu, naye Mathieu Debuchy ataingia nafasi ya Hector Bellerin.

Kiungo wa kati Jack Wilshere na mshambuliaji Danny Welbeck wako nje kwa muda mrefu baada ya kufanyiwa upasuaji Septemba. Viungo wa kati Aaron Ramsey, Mikel Arteta naTomas Rosicky pia wako nje kutokana na majeraha.

Meneja Arsene Wenger lazima aamue iwapo atamtumia Joel Campbell baada ya raia huyo wa Costa Rican kufunga mechi yake ya kwanza kabisa kuanza katika Ligi ya Premia dhidi ya Swansea Jumamosi.

Ushindi wa Arsenal dhidi ya Bayern mechi ya mkondo wa kwanza ilikuwa ya kwanza kabisa kwa mabingwa hao wa Ujerumani kushinda katika mechi 21 msimu huu.

Walihitaji sana ushindi huo wanapojaribu kuwa timu ya kwanza tangu Galatasaray mwaka 2012-13 kuhusu kwa hatua ya muondoano baada ya kushindwa mechi mbili za kwanza katika kundi, mikononi mwa Dinamo Zagreb na Olympiakos.