Van Gaal: Waacheni wachezaji, nizomeeni mimi

Haki miliki ya picha PA
Image caption Van Gaal amesema huenda baadhi ya wachezaji wanaathiriwa na shinikizo za mashabiki

Meneja wa Manchester United Louis van Gaal amewaambia mashabiki wamzomee yeye badala ya wachezaji.

Hii ni baada ya baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo ya Old Trafford kuitaka timu hiyo icheze mchezo wa kushambulia zaidi.

United wamefunga bao moja pekee katika mechi zao nne za majuzi zaidi na mashabiki waliimba “tunataka kushambulia” wakati wa ushindi wao mwembamba wa 1-0 dhidi ya CSKA Moscow Jumanne.

“Ninaweza tu kuwashauri mashabiki wamkosoe meneja na si wachezaji,” amesema.

“Mimi ninaweza kukabiliana na ukosoaji. Nimepitia mengi maishani mwangu kama meneja.”

Van Gaal ameongeza kuwa mazingira Old Trafford huenda yakawa yanaathiri uchezaji wa timu yake.

"Ni vigumu sana kuchezea Manchester United ukikabiliwa na presha sana na unaweza kuhisi hilo Old Trafford kwa sababu ya kelele za mashabiki, hili si jambo njema kwa wachezaji wangu,” amesema.

Manchester United watakutana na West Brom uwanjani Old Trafford Jumamosi.

West Brom wameenda mechi nne kati ya tano walizocheza ugenini Ligi ya Premia msimu huu bila kufungwa bao lolote.