Ripoti yapendekeza Urusi izuiwe kushiriki riadha

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Diack anachunguzwa kwa tuhuma za ulaji rushwa

Ripoti ya uchunguzi huru kuhusu madai ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli miongoni mwa wanariadha Urusi imependekeza taifa hilo lizuiwe kushiriki michezo ya IAAF.

Tume huru, iliyoundwa na shirika la kukabiliana na matumizi ya dawa zilizoharamishwa (Wada), imesema kulikuwa na makosa mengi katika ufuatilizi wa sheria kuhusu matumizi ya dawa zilizoharamishwa.

Imependekeza pia rais wa zamani wa shirikisho la riadha duniani IAAF Lamine Diack asimamishwe kutoka kwa mchezo wa riadha, ikisema alihusika katika kuficha kuhusika kwa wanariadha wa Urusi katika kutumia dawa za kusisimua misuli.

Diack tayari anachunguzwa na polisi Ufaransa kwa madai ya kupokea zaidi ya euro 1 milioni kuficha uhalifu huo.

Mwanawe Papa Massata Diack, mshauri wake Habib Cisse na mkuu wa zamani wa kupambana na matumizi ya dawa zilizoharamishwa katika IAAF Gabriel Dolle

Lord Coe, rais wa sasa wa IAAF amekiri kwamba hizi ni “siku za giza kwa mchezo huo”.

Kwenye mahojiano na BBC Radio 5 Coe ameongeza: "Siku moja baada yangu kuchaguliwa, nilianzisha utathmini mkubwa. Kutokana na madai ambayo yametolewa, utathmini huu umeharakishwa.

“Nimejitolea sana kurejesha Imani katika mchezo huu. Hata hivyo, hii ni safari ndefu.”

McLaren, mmoja wa waliochangia kuandika ripoti hiyo, alikuwa awali ameambia BBC World Service kwamba tume hiyo huru ilikuwa na jukumu la kubaini ukweli kuhusu madai yaliyotolewa kwenye makala moja ya televisheni ya Ujerumani kuhusu wanariadha wa Urusi mwezi Desemba.

Makala hiyo ilidai maafisa wa Urusi walipokea pesa kutoka kwa wanariadha ili kuwapa dawa zilizoharamishwa na kuficha ukweli wakati wa kupimwa kwao. Maafisa wa IAAF walihusika katika kuficha ukweli.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Coe amekiri hizi ni siku za giza kwa mchezo wa riadha

Coe, anayetoka Uingereza, alikuwa makamu wa rais wa shirikisho hilo kwa miaka minane kati ya 16 ambayo Diack alikuwa kwenye usukani.

Hata hivyo amesema hakufahamu lolote kuhusu tuhuma zilizowasilishwa dhidi ya raia huyo wa Senegal, aling’atuka Agosti, hadi zilipotangazwa hadharani mwanzoni mwa wiki iliyopita.

“Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kuyasikia madai hayo na nina uhakika hata kwa watu wengi katika mchezo huu ni vivyohivyo.”

Wakati wa kuchaguliwa kwake, Coe aliyeshinda Olimpiki mbio za 1500m mara mbili alimtaja Diack kama “kiongozi wa kidini wa IAAF lakini alikiri Jumapili kwamba huenda akashutumiwa kwa madai hayo.

Hata hivyo alisema: “Lakini huko ni kudhani kwamba nilifahamu tuhuma hizi zozote nikisema hayo, jambo ambalo si kweli.