Timu ya Kenya yakwama kwa sababu ya hela

Harambee
Image caption Harambee Stars walishinda 1-0 mechi ya mkondo wa kwanza

Timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars imekwama uwanja wa ndege wa Wilson kufuatia mzozo kuhusu marupurupu na malipo.

Timu hiyo ilikuwa imepangiwa kufunga safari ya saa tisa kuelekea visiwa vya Cape Verde kucheza mechi ya marudiano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia Urusi 2018.

Mechi hiyo inatarajiwa kuanza kesho saa nne usiku saa za Afrika Mashariki.

Lakini safari yao ilicheleweshwa baada ya wachezaji kutaka walipwe marupurupu na warejeshewe nauli ya kusafiri hadi Nairobi kabla yao kukubali kuabiri ndege.

Maafisa wakuu serikalini waliingilia kati na wakalipwa lakini baadaye kampuni ya kukodisha ndege waliyopangiwa kusafiria nayo inadaiwa kutaka ilipwe pesa zote kabla ya ndege kupaa kuelekea mjini Praia.

Harambee Stars walishinda mechi ya mkondo wa kwanza Nairobi 1-0 Ijumaa iliyopita.