Tanzania bara kuchuana na wenyeji Ethiopia

Image caption Cecafa

Hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge inahitimishwa leo kwa michezo miwili.

Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' itamenyana na wenyeji, Ethiopia mjini Awassa katika mchezo wa Kundi A na Uganda itapambana na Burundi katika mchezo wa Kundi B.

Kili Stars hadi sasa imejihakikishia hatua ya robo Fainali baada ya ushindi mfululizo katika mechi mbili za awali, 4-0 dhidi ya Somalia na 2-1 dhidi ya Rwanda na leo inakamilisha mechi zake za Kundi A ikiwa kileleni.

Image caption Cecafa

Mechi nyingine za mwisho za makundi zilichezwa jana, Zanzibar ikiifunga Kenya mabao 3-1, wafungaji, Suleiman Kassim 'Selembe' mawili na Khamis Mcha 'Vialli' moja, wakati bao la Harambee Stars lilifungwa na Jacob Keli, Rwanda imeifunga 3-0 Somalia, wakati Sudan Kusini iliifunga 2-0 Malawi,Sudan iliifunga Djibouti 4-0.