Kilimanjaro Stars ya Tz kurejea leo

Image caption Kikosi cha Kilimanjaro Stars cha Tanzania

Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kinatarajiwa kuwasili leo mchana jijini Dar es salaam kikitokea nchini Ethiopia kilipokuwa kinashiriki michuano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Kilimanjaro Stars imetolewa katika hatua ya robo fainali na wenyeji Ethiopia kwa mikwaju ya penati, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za mchezo huo, na wenyeji kushinda kwa penati 4-3.

Katika michezo wa makundi, Kilimanjaro iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Somalia, ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Rwanda, na sare ya bao 1-1 dhidi ya Ethiopia.

Baada ya kurejea nyumbani,chama cha soka TFF kwa kushirikiana na benchi la ufundi wataanza maandalizi ya michezo dhidi ya Chad itakayochezwa Machi 2016 kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2017.